Na Albano Midelo - Songea
...............................................................
WILAYA ya Nyasa mkoani Ruvuma bado ina fursa za maliasili ya kutosha zikiwemo misitu, wanyamapori, samaki, mito, ziwa, fukwe na mali kale ambazo hazijaharibiwa ndiyo maana tunasema wilaya ya Nyasa ni benki ya vivutio vya utalii na uwekezaji.
...............................................................
WILAYA ya Nyasa mkoani Ruvuma bado ina fursa za maliasili ya kutosha zikiwemo misitu, wanyamapori, samaki, mito, ziwa, fukwe na mali kale ambazo hazijaharibiwa ndiyo maana tunasema wilaya ya Nyasa ni benki ya vivutio vya utalii na uwekezaji.
Moja ya kivutio adimu cha utalii katika wilaya ya Nyasa ni uwepo wa Ziwa Nyasa ambalo ni la tisa kwa ukubwa duniani,ni la tatu kwa ukubwa barani Afrika.
Ziwa hilo lina kina cha kati ya mita 426 na 758 na hii ni kutokana na kupitiwa na bonde la ufa. Kwa upande wa Tanzania mito mingi inapatikana ikitokea wilaya ya Nyasa katika safu za milima ya Livingstone, mito hiyo ni Ruhuhu, Lumeme, Ruhekei, Lwika,Mbamba Bay,Likumbo na Chiwindi ambayo huingiza maji ndani ya Ziwa Nyasa.
Kwa mujibu wa Afisa Maliasili na Utalii wa wilayani Nyasa,ziwa Nyasa ni kuvutio kikubwa cha Utalii kanda ya kusini kwa kuwa limesheheni vitu vingi ndani yake na tabia tofauti ukilinganisha na maziwa mengine ya hapa nchini na duniani kote.
“Baadhi ya tabia za ziwa hili ni uwepo wa maji meupe na maangavu eneo lote la ziwa na mawe marefu ambayo yanajulikana kwa majina ya hiana mala yanayobeba sifa tofauti’’,anasema Bugingo.
Kulingana na ripoti ya utafiti wa mwaka 2011,asilimia 15 ya aina za samaki wa maji baridi duniani wanapatikana ziwa Nyasa ambapo kuna aina ya samaki tofauti zaidi ya 600,huku kukiwa aina ya samaki wa mapambo zaidi ya 400 na viumbe wengine ambao hawapatikani katika ziwa lolote duniani wanapatikana katika maeneo tofauti ndani ya ziwa Nyasa kutegemeana na aina na usalama wa maisha yao.
Jonathan Ruanda Mtaalam wa kuzamia samaki wa mapambo katika ziwa Nyasa na Mfanyabiashara wa samaki hao anasema tangu mwaka 1960 samaki hai wa mapambo toka ziwa Nyasa walianza kuuzwa katika nchi za Ulaya na Marekani.
Hata hivyo anasema nchi nyingi kama vile Japani, Swedeni, Uturuki, Denmark, Canada, Ufaransa, Uingereza na Ujerumani zilivutiwa na samaki wa mapambo kutoka ziwa Nyasa kutokana na kuwa na sifa ya kipekee yaani rangi nzuri za kupendeza na hakuna sehemu nyingine wanapatikana samaki wa mapambo wa aina hii.Mbunge wa Jimbo la Nyasa na Naibu Waziri wa Viwanda,Biashara na Uwekezaji Mhandisi Stella Manyanya anabainisha kuwa Ziwa Nyasa pia limesheheni utajiri mkubwa wa viumbe hai wakiwemo fisimaji, mamba, nyoka na viboko ambao ni kivutio kikubwa cha utalii.
“Ndege wanaohamia kutoka Ulaya na baadhi ya nchi za Afrika wanapatikana maeneo ya mwambao mwa ziwa Nyasa ambao ni kivutio kikubwa cha utalii’’,anasisitiza Mhandisi Manyanya.
Manyanya anasema Nyasa imejaliwa utalii wa aina karibu zote ndiyo maana eneo hilo linaitwa ni Benki ya vivutio vya utalii ambavyo bado havijatangazwa kikamilifu ili kuwa moja ya chanzo cha mapato.
No comments:
Post a Comment